Tuesday 19 July 2016

AINA ZA NYUKI NA TABIA ZAO.



Nyuki ni jamii ya wadudu wenye jozi mbili za mabawa mepesi yenye mishipa laini.Nyuki huishi maisha ya kijamaa. Mwili wa Nyuki umegawanyika katika sehemu kuu tatu; kichwa, kifua na tumbo(fumbati). Tofauti na wadudu wengine, nyuki hutengeneza na kuhifadhi Asali kwenye masega.Kuna takribani aina tofauti elfu ishirini(20,000) Duniani. Nyuki hawa wanatofautiana kwa maumbile, ukubwa na tabia, lakini wote wanashahabiana kwa tabia moja ya kutembelea maua ili kukusanya mbochi(maji matamu yanayotengeneza asali) na chavua(unga unaopatikana kwenye maua) kwa ajili ya chakula chao.Kuna jamii kuu mbili za Nyuki wanaopatikana Tanzania; Nyuki wanaouma na wasiouma.


NYUKI WANAOUMA.


Nyuki wanaouma wanaopatikana Tanzania, wamegawanyika katika makundi matatu kutegemea mahali wanapoishi.Wapo nyuki wanaoishi;Sehemu za Mwambao(Pwani) wana umbo dogo ni wakali (Apis mellifera litorea), sehemu kame, tambarare, wana umbo la wastani, wakali kiasi na hutoa asali kwa wingi (Apis mellifera scutellata), sehemu za milimani, (zaidi ya futi 6,000 kutoka usawa wa Bahari) wana umbo kubwa na wapole, jina la kitaalamu wanaitwa (Apis mellifera monticola).


NYUKI WASIOUMA.


Nyuki wasiouma wanapatikana nchi za tropiki tu kama ilivyo Tanzania.Nyuki wasiouma wanaishi ndani ya matundu ya miti, chini ya matawi makubwa ya miti, kwenye vichuguu vya mchwa na hata chini ya mapaa ya nyumba, nyuki hawa hutoa asali kidogo kulinganisha na nyuki wanaouma. Nyuki wasiouma wanaweza kutoa hadi lita 5 za asali kwa mwaka kutegemea na ukubwa wa mzinga, aina, wingi wa nyuki na uwepo wa chakula(maua) cha kutosha. Asali ya Nyuki wasiouma inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kutibu maradhi mbalimbali kuliko asali ya Nyuki wanaouma.







JINSIA ZA NYUKI NA MAJUKUMU YAO.


Kama ilivyo kwa viumbe vyote, nyuki nao wana jinsia mbili, Nyuki Dume na Nyuki Jike. Jinsia hizo ndiyo msingi wa mgawanyo wa majukumu ya kazi katika kundi la Nyuki.Kundi la Nyuki wanaouma lina aina tatu za Nyuki ambao ni Nyuki Vibarua, Malkia na Dume.


a)Nyuki Malkia


Ni nyuki jike ambaye hulelewa kwa kula chakula rasmi (maziwa ya Nyuki) na kupata matunzo maalumu kwa maisha yake yote (tangu hatua ya yai hadi uzee wake wote) Chakula hiki humwezesha kuishi kati ya miaka miwili hadi sita.Nyuki Malkia ni mkubwa kuliko nyuki wengine katika kundi la Nyuki, tumbo lake ni refu lenye rangi ya njano na dhahabu ghafi.Nyuki Malikia, hutoa kemikali (Pheremones) mwilini mwake kutoa miongozo kwa kundi la Nyuki.Mpangilio wote na mgawanyo wa kazi katika kundi la nyuki hutegemea maelekezo yake. Kundi la Nyuki lisilo na Malkia hukosa mwelekeo na huishi kwa kipindi kifupi.


b)Nyuki Vibarua


Nyuki Vibarua ni majike ambao maumbile yao hayana uwezo wa kutaga mayai wala kujamiiana na nyuki madume. Kwa kawaida Nyuki Vibarua ambao hawatagi mayai ni majike tasa ambao hawana uwezo wa kutaga mayai. Aidha,hufikia kuishi hadi siku 36. Wanaweza kufikia idadi ya 60,000 au zaidi katika kundi moja.


c)Nyuki dume


Hutokana na mayai ya  Nyuki Malkia yasiyorutubishwa na mbegu za kiume na kuwafanya nyuki hao kuwa na mzazi mmoja tu yaani mama, Nyuki Dume ni wakubwa kuliko Nyuki Vibarua lakini wadogo kuliko Nyuki Malkia. Macho yao ni makubwa na miili yao ina rangi nyeusi, Nyuki Dume hawana mshale wa sumu kwa ajili ya kujilinda dhidi ya maadui, badala yake wana uume.Kazi kubwa ya Nyuki Dume ni kujamiiana na Nyuki Malkia. Nyuki Dume mmoja huweza kujamiiana na Nyuki Malikia mara moja katika maisha yake. Baada ya Tendo la kujamiiana yeye hufa saa chache kutokana na uume wake kukatika wakati wa kujamiiana. Kwa hali hii hata Nyuki Vibarua hawajawai kuwaona baba zao.!Kazi ya pili ya Nyuki Dume ni kurekebisha hali ya hewa ndani ya mzinga kwa kupasha joto kiota hasa wakati wa Usiku kwa kukumbatia juu ya kiota na sehemu ya watoto. Wakati wa upungufu mkubwa wa chakula au kiangazi Nyuki Dume hutolewa nje ya mizinga na Nyuki Vibarua na baadea hufa kwa njaa au baridi.


Spishi na Nusu-spishi za Afrika
Apis mellifera
Apis m. adansonsii   (Nyuki-asali wa Adanson)
Apis m. capensis   (Nyuki-asali kusi)
Apis m. intermissa (Nyuki-asali mweusi)
Apis m. jemenitica  (Nyuki-asali wa Pembe la Afrika)
Apis m. lamarckii  (Nyuki-asali wa Lamarck)
Apis m. litorea  (Nyuki-asali pwani)
Apis m. major  (Nyuki-asali wa Maroko)
Apis m. monticola  (Nyuki-asali milimani)
Apis m. nubica  (Nyuki-asali wa Sudani)
Apis m. sahariensis  (Nyuki-asali jangwani)
Apis m. scutellata  (Nyuki-asali wa Afrika)
Apis m. unicolor  (Nyuki-asali wa Madagaska).


Spishi za Asia
Apis florea (Red Dwarf Honey Bee)
Apis andreniformis (Black Dwarf Honey Bee)
Apis dorsata (Giant Honey Bee)
Apis cerana (Asiatic Honey Bee)
Apis nigrocincta (Philippine Honey Bee).

No comments:

Post a Comment