Wednesday 20 July 2016

NYUKI

Mzinga wa Nyuki

Ufugaji wa NYUKI unaweza kuwa chanzo kizuri cha kipato kwa Wakulima.

Uzalishaji wa asali nchini Tanzania umekuwa ukitegemea sana wafugaji wadogo wadogo, wanaotumia njia za kiasili kama vile mizinga ya magogo au vyungu, kwa nyuki wa kiafrika ambao ni wengi sana kwenye mapori.

Ni muhimu kuwa na utaalamu wa kufuga nyuki.
Mkulima ambae anahitaji kufuga nyuki ni lazima awe na uelewa wa mzunguko wa maisha ya nyuki. Anaye anza ni lazima aulize wafugaji wenzake ambao wana uzoefu wa kutosha, au kujiunga katika kikundi cha ufugaji ili apate ufahamu zaidi juu ya ufugaji wa nyuki.

Tafuta sehemu salama kwa ajili ya mzinga
Ni vizuri kutafuta mahali pazuri, salama, na penye sifa ya kufugia nyuki. Vifaa vyote vikishapatikana jambo linalofuata ni kuchagua mahali gani pa kuweka mzinga. Ni vizuri sehemu hii ikawa mahali ambapo makundi ya nyuki hukusanyika mara kwa mara. Mara nyingine kupata eneo sahihi ni tatizo.

Ni vizuri kuzingatia yafuatayo:
ü  Kulingana na hali ya kujilinda ya nyuki wa Afrika, haishauriwi kuweka mzinga shambani au karibu na shamba (weka umbali wa mita 150-200 kutoka kwenye mazao au nyumbani)
ü  Mzinga ni lazima uwekwe sehemu ambayo haitasababisha upotevu wa nyuki wanaporudi kutoka nje ya mzinga (wasiingie kwenye kundi lisilokuwa lao)
ü  Mizinga isiwekwe mbalimbali sana ili kuepusha usumbufu wa kutembea mbali kwa mfugaji wakati anapokagua.

Eneo la kuweka mizinga ni lazima liwe :
ü  Kimya, mbali na jumuia (hospitali, shule, na viwanja vya michezo) na maeneo ya biashara au viwanda.
ü  Karibu na maji masafi-kandokando ya mto, mabwawa ya samaki, mabeseni ya maji au sehemu ya matone.
ü  Iwe karibu na chakula cha nyukimimea inayochanua, miparachichi,
ü  nazi, euculptus, migunga n.k
ü  Iwe sehemu ambayo ni kavu na isiwe sehemu ya tindiga kwani unyevu unyevu husababisha ugonjwa wa ukungu (fungal disease) na pia huzuia utengenezaji mzuri wa asali.
ü  Iwe mbali na watu waharibifu na iliyojificha kuepuka waharibifu.
ü  Sehemu ya mizinga ni lazima iwe inafikika kirahisi kwa kipindi chote cha mwaka ili iwe rahisi kuhamisha nyuki pale inapohitajika.
ü  Kuwe na kivuli cha kutosha hasa wakati wa mchana jua linapokuwa kali, na kusiwe na upepo mkali.
ü  Iwe mbali na mashamba, ambapo dawa za kuulia wadudu zinatumika.
ü  Vichaka au wigo unaotenganisha mizinga na kuzuia wavamizi ni muhimu ili kupunguza ukali wa nyuki. 

Jinsi ya kuweka mzinga.
Baada ya sehemu ya kuweka mizinga kupatikana, kinachofuata ni kuandaa mizinga kwa ajili ya kuweka panapotakiwa.

ü  Safisha mzinga kuondoa uchafu wote, utando wa buibui na aina nyingine za wadudu.
ü  Weka chambo kwenye mzinga (wafugaji wa nyuki mara nyingi hutumia NTA) kwa kuipaka katika kuta za mzinga kwa ndani.
ü  Mzinga unaweza kutundikwa kwenye mti, kwenye nguzo, kuweka kwenye jukwaa au kwenye miamba. Hii inategemea mkulima mwenyewe anapendelea njia ipi.

No comments:

Post a Comment