Thursday 8 September 2016

MAKALA KUHUSU PARACHICHI NA USINDIKAJI WAKE.

Maparachichi ni moja ya zao la matunda ambalo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mbeya,
Kilimanjaro, Morogoro, Kigoma, Kagera, Arusha na Tanga. Wastani wa uzalishaji ni tani 5574.4 kwa mwaka. Zao hili ni muhimu katika lishe kwani lina mafuta na protini kwa wingi kuliko matunda yote yanayoliwa nchini.


MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA UZALISHAJI
Ili kupata matunda yenye ubora unaotakiwa ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo bora za
uzalishaji wa maparachichi. Hii ni kwa sababu ubora wa mazao baada ya kuvunwa
hutegemea jinsi mazao hayo yalivyozalishwa. Baadhi ya kanuni za kuzingatia ni kama
zifuatazo:
  • Chagua aina bora kupanda kulingana na mahitaji ya soko.
  • Dhibiti magonjwa na wadudu ili kupata mazao mengi na bora yanayoweza kuhifadhiwa kwa
    muda mrefu.
  • Pia dhibiti magugu na safisha barabara ndani ya shamba ili kurahisisha kazi ya kuvuna na kusafirisha mazao.
MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA
  • Maandalizi yanayotakiwa kabla ya kuvuna ni kama yafuatayo:


Kukagua shamba.
  • Kagua shamba ili kuona kama matunda yamekomaa.
  • Kwa kawaida maparachichi hukomaa katika kipindi cha miezi sita hadi tisa kutoka maua yanapochanua.
Dalili za maparachichi yaliyokomaa.
Si rahisi kutambua maparachichi yaliyokomaa kwa kuangalia rangi ya tunda. Hivyo ni muhimu kuzingatia muda wa kukomaa. Maparachichi yakivunwa yangali machanga hunyauka na kuoza. Ni vyema kuchuma parachichi moja au mawili na kuyakata kuona rangi yake kwa ndani ambayo itadhihirisha kukomaa kwa matunda.


KUANDAA VIFAA, VYOMBO VYA KUVUNIA, KUFUNGASHIA NA KUSAFIRISHIA.
  • Ngazi
  • Vikapu
  • Vichumio
  • Makasha ya mbao
  • Mifuko
  • Matenga
  • Matoroli
  • Magari
  • Baiskeli
  • Matela ya matrekta.
KUVUNA.
Njia bora ya kuvuna ni kutumia Mikono.
  • Kwa miparachichi mifupi chuma tunda pamoja na kikonyo chake kwa kutumia mkono.
  • Kwa miparachichi mirefu chuma matunda kwa kutumia kichumio maalum au kwea mti kwa
    kutumia ngazi na chuma kwa mkono.
  • Chuma matunda yaliyokomaa tu. Uvunaji wa matunda ambayo hayajakomaa husababisha matunda kusinyaa na nyama ya ndani kuwa na kambakamba wakati wa kuivisha.
  • Acha kikonyo chenye urefu wa sentimeta moja kwenye tunda
  • Vuna wakati wa asubuhi au jioni ili kuepuka jua kali linaloweza kubabua matunda.
  • Weka kwenye sehemu yenye kivuli. Jua hubabua matunda na huongeza kasi ya kuoza.
  • W akati wa kuvuna hakikisha matunda hayadondoki chini.
Kuchambua, Kusafisha na Kupanga Madaraja.
Shughuli ya kuchambua, kusafisha na kupanga madaraja ifanyike kivulini ili kuepuka jua
ambalo linaweza kubabua matunda.

Kuchambua.
Ni muhimu kuchambua maparachichi ili kutenga yaliyoshambuliwa na wadudu, magonjwa na yaliyopasuka au kuchubuka au yenye makovu.
  • Matunda yaliyooza na yenye wadudu hayafai kwa matumizi hivyo yafukiwe, ili kuepusha ueneaji wa magonjwa.
  • Matunda yaliyopasuka, kuchubuka kidogo au kubonyea yatumike haraka.
  • Matunda mazuri ambayo hayajapata madhara yoyote yawekwe kwa ajili ya kusindikwa, kutumika au kuuzwa.
Kusafisha.
Baada ya kuchambua maparachichi yaoshwe kwa maji safi ili kuondoa uchafu na masalia
ya madawa.

Kupanga madaraja.
  • Kabla ya kupanga madaraja ni muhimu kupunguza vikonyo vya matunda. Punguza na ubakize vikonyo vyenye urefu wa milimita tano. Vikonyo virefu zaidi kufanya ufungashaji kuwa mgumu.
  • Upangaji wa madaraja hufuata uzito na ukubwa wa matunda.
  • Tenganisha matunda yaliyoharibika umbo, yaliyochubuka au yaliyoiva kupita kiasi, au yenye makovu.
  • Inashauriwa kunyunyiza nta kwenye maparachichi ili kupunguza upotevu wa maji, kurefusha muda wa kuhifadhi na kufanya yavutie kwenye soko.
Kufungasha.
Vifungashio vinavyotumika kufungashia maparachichi ni kama vilivyoonyeshwa hapo juu,
baahdi yake ikiwa ni:
  • Makasha ya mbao
  • Matenga--Ufungashaji wa kwenye matenga yaliyosukwa vizuri ili kuruhusu hewa kupita yanatumika katika ubebeaji wa mboga na matunda. Inashauriwa kupanga bidhaa vizuri ndani ya matenga hayo baada ya kutanguliza vitu visafi kama makaratasi au nyasi safi na kavu au majani safi na makavu ya migomba ili kuzuia michubuko ya matunda yanapogongana. Vifaa vya kutanguliza kwenye vifungashio lazima viwe safi, visivyoingiza vimelea vya ugonjwa kwenye matunda.

Kusafirisha.
Baada ya kufungasha matunda, inashauriwa kupanga vizuri ndani ya vyombo vya usafiri na
kutozidisha ujazo kwenye vyombo hivyo ili kuepusha upoteaji unosababishwa na kumwagika au kupasuka kwa matunda na kuchubuka. Barabara nyingi za vijijini sio za lami na ujazo mkubwa wa vifungashio ndani ya magari ya kusafirisha mazao hadi mijini husababisha upotevu mkubwa wa mboga na matunda. Vilevile uangalifu unahitajika wakati wa kupakia na kupakua.

Kuhifadhi.
  • Maparachichi huweza kuhifadhiwa kwenye joto lipatalo nyuzi 10 hadi 18 za Sentigredi ambapo hudumu kwa kipindi cha wiki tatu bila kuharibika.
  • Matunda yakihifadhiwa kwenye nyuzi joto 20 hadi 25 za Sentigredi huiva haraka na huhifadhika katika muda mfupi (siku 5 hadi 15).
KUSINDIKA MAPARACHICHI.

Kusindika maparachichi kupata Guakamole.
Vifaa;-
  • • Mashine ya kusaga rojo
    • Bakuli ya kuoshea maparachichi
    • Kisu kikali kisichoshika kutu.
    • Chupa za kufungashia zenye mifuniko imara
    • Lebo
Malighafi;-
  • Maparachichi mawili
  • Kitunguu maji kimoja.
  • Pilipili kali moja.
  • Juisi ya limao kidogo.
  • Giligilani ya majani 25.
  • Chumvi na pilipili manga kidogo.
  • Maji safi na salama.
  • Nyanya moja kubwa.
Jinsi ya kutengeneza;-
  • • Menya kitunguu,
    • Kata kitunguu na pilipili kali,
    • Osha maparachichi na giligilani,
    • Saga giligilani kwenye mashine ya kusaga,
    • Ongeza maparachichi, juisi ya limao, nyanya, pilipili, kitunguumaji. Chumvi na pilipili manga,
    • Saga hadi mchanganyiko uwiane,
    • Fungasha guakamole kwenye chupa za kioo,
    • Weka lebo,
    • Hifadhi mahali penye baridi.
Matumizi;-
  • Hutumika kama sosi baridi pamoja na vitafunwa kam mikate au pamoja na mboga za majani.
  • Hutumika kama saladi (mchanganyiko wa matunda)
  • Hutumika ikiwa katika hali ya kusindikwa. Bidhaa inayotokana na parachichi ni “guakamole” ambayo hutumika pamoja na chipsi au chakula chochote kilichotengenezwa kutokana na nafaka.
VIRUTUBISHO.
Virutubishi vinavyopatikana kwenye gramu 100 za maparachichi
  • Maji gramu 72
  • Mafuta gramu 21.8
  • Wanga gramu 6
  • Nguvu kilokalori 875
  • Kalsiamu miligramu 10
  • Fosiforasi miligramu 34
  • Vitamini A I.U 800
  • Vitamini C miligramu 15

2 comments: