Zao hili hustawi katika joto la wastani, na hukua kwa
haraka zaidi na uzalishaji kuongezeka linapolimwa kisasa, hasa katika nyumba
maalumu ya kuzalishia mimea yaani green house. Zao hili hukua vizuri katika
mwinuko wa mita 1500 kutoka usawa wa bahari. Endapo unahitaji kuzalisha
stroberi katika maeneo ya bondeni
itakulazimu kuwa na maji kwa wingi kwa ajili ya umwagiliaji wa mara kwa mara.
Udongo
Stroberi inaweza kustawi vizuri kwenye udongo tifutifu
wenye rutuba. Zao hili haliwezi kustahimili ukuaji kwenye udongo wenye chachu
nyingi, hasa chokaa kwani mizizi yake huoza kwa urahisi.
Kupanda
Ili kuwa na mazao bora ambayo yatakuwezesha kupata soko
la uhakika, bila vipingamizi, inashauriwa kuzalisha kwenye nyumba maalumu ya
kuzalishia mazao (green house). Katika kuzalisha stroberi baada ya kujenga green
house andaa mabomba ya plastiki ambayo yatawezesha kutoboa matundu kwa
urahisi (tazama picha).
• Matundu katika bomba hilo yawe na umbali wa inchi 1.
• Ni vyema matundu hayo yakawa zigizaga, ili kuruhusu
mimea utakayopanda kukua vizuri bila kuwekeana kivuli.
• Tandika karatasi la nailoni sakafuni ili kuwezesha maji
utakayotumia kunyeshea kurudi kwenye bwawa au sehemu ya kuhifadhia.
• Ning’iniza mabomba hayo kwa kutumia waya.
• Jaza kokoto, yenye mapande makubwa kiasi.
• Panda miche kwenye kila tundu kwa uangalifu ili mizizi
isikatwe na kokoto zinazoshikilia mmea.
Kumwagilia
Mimea ya stroberi inahitaji maji kwa kiasi kikubwa sana.
Hii inamaanisha kuwa unahitaji kuwa na mfumo mzuri wa umwagiliaji kabla ya
kuanza kilimo cha zao hili. Unapaswa kumwagilia mara nne kwa siku, kila baada
ya saa nne unapaswa kumwagilia kwa robo saa. Hii itawezesha mimea yote kupata maji
ya kutosha. Endapo stroberi haitapata maji ya kutosha, uzalishaji wake pia utakuwa
ni hafifu sana, kwani maua hayatachanua ipasavyo na hata matunda kukomaa
inakuwa ni shida.
Mbolea
Uzalishaji wa kisasa wa stroberi, unaambatana na ufugaji
wa samaki kwenye bwawa ndani ya green house. Mbinu hii husaidia mimea
kupata mbolea inayotokana na chakula wanacholishwa samaki kwenye bwawa, kwani
maji yanayofugia samaki ndiyo hayo yanayotumika katika mzunguko wa umwagiliaji.
Hii inamaanisha kuwa hakuna mbolea nyingine inayohitajika kwa ajili ya
stroberi.
Wadudu na magonjwa
Endapo stroberi inazalishwa kwenye nyumba maalumu ya
mimea, hakuna magonjwa wala wadudu wanaoishambulia. Ikiwa mkulima anazalisha
stroberi kwenye eneo la wazi, stroberi inaweza kushambuliwa na magonjwa ya ukungu,
pamoja na magonjwa yanayosababishwa na virusi.
Dawa
Endapo stroberi itashambuliwa na magonjwa ya ukungu na
virusi, nyunyizia dawa za asili kama vile pareto na mwarobaini, na baada ya
muda kutakuwa na matokeo mazuri.
Kuvuna
Zao la stroberi, huzaliana na kukomaa kwa haraka sana.
Unaweza kuanza kuvuna stroberi baada ya mwezi mmoja tangu kupandwa. Kila wiki
stroberi inakuwa na matunda mapya, na kila tunda likishatokeza huiva kwa
haraka, hivyo uvunaji wake ni wa mfululizo. Ikishafikia hatua hiyo tegemea kuwa
na wiki 2-3 za kuvuna mfululizo. Kwa kuwa matunda ya stroberi ni laini, epuka
kushika tunda wakati wa uvunaji ili lisiharibike. Shika kikonyo cha tunda ili
kuvuna kwa usalama. Usiache matunda yaliyoiva shambani kwa muda mrefu kwani
yanaweza kusababisha mimea kuoza. Pia yatapoteza ladha na virutubisho halisi
vinavyotakiwa.
Virutubisho
Stroberi ina kiasi kikubwa cha virutubisho hasa vitamin
B, C, K, na E . Pia yana wingi wa madini ya chumvi. Matunda haya husaidia
kuchangamsha mwili na yana kiasi kidogo cha kalori.
Matumizi ya stroberi
Matunda ya stroberi yana matumizi mbalimbali kulingana na
uhitaji wa mtumiaji, jamii na maeneo. Miongoni mwa matumizi hayo ni pamoja na:
• Kuliwa kama tunda.
• Kutia ladha katika aina mbalimbali za vyakula.
• Kuweka rangi, harufu na nakshi katika vipodozi.
• Kutengeneza marashi n.k.
Soko na bei
Stroberi ina soko zuri kulingana na ubora wake. Kwa sasa
gramu 50 za stroberi zinauzwa kati ya shilingi 5,000-10,000 za kitanzania.
No comments:
Post a Comment