Mbaazi ni zao
jamii ya mikunde inayostawi katika nchi za kitropiki zenye mvua chache. Zao
hili ni muhimu sana kwa nchi za Asia ambako ni mojawapo ya chakula kikuu hasa
katika nchi ya India.
Kwa miaka ya hivi karibuni, zao la mbaazi limekuwa moja ya mazao muhimu
ya biashara katika maeneo mengi ulimwenguni. Hii ni kutokana na ongezeko la walaji
na uwezo wake wa kustahimili ukame na mvua chache ambao unaendana na mabadiliko
ya hali ya hewa ulimwenguni kote. Nchini Tanzania, zao hili hulimwa kwa wingi
katika mikoa ya Manyara (Hanang na Mbulu), Arusha (Arusha vijijini na Meru),
Dodoma (Kondoa), Kilimanjaro (Same, Mwanga, Rombo, Hai na Moshi vijijini)
Mbaazi kwa kawaida hupandwa kwa msimu mmoja lakini aina za kienyeji zinaweza
kulimwa kama zao la kudumu ambapo huweza kukaa shambani miaka mitatu hadi
mitano ingawa uzalishaji wa mazao hupungua msimu hadi msimu.
Matumizi ya Mbaazi
Chakula/mboga hasa
zikiwa mbichi. Mbaazi mbichi huwa na protini zaidi ya asilimia 21%, wanga
asilimia 44.8%, mafuta asilimia 2.3% pamoja na baadhi ya virutubisho vya madini
kama chokaa na chuma.
Zao la biashara.
Kutokana na kuwepo kwa aina bora za mbaazi zinazohitajika kwa wingi katika soko
la ndani na nje pamoja na kuwepo kwa aina zinazokomaa mapema na kuwahi soko la
dunia, zao hili limekuwa likilimwa kwa ajili ya biashara hasa katika wilaya za
Babati, Karatu, Arumeru pamoja na Kondoa
Chanzo cha nishati
(kuni). Miti ya mbaazi hutumiwa kwa ajili ya kuni katika maeneo ya ukanda
wa chini ambayo haina miti. Matumizi haya pia husaidia kupunguza uharibifu wa
mazingira kutokana na watu kutokukata miti ovyo.
Kirutubisho cha
udongo. Mbaazi ni jamii ya mikunde ambayo huongeza mbolea aina ya
Naitrojeni kwenye udongo. Majani yake yanapopukutika na kudondoka ardhini huoza
na kubadilika kuwa mbolea ambayo pia huboresha muundo wa udongo. Chakula cha
mifugo. Maganda na majani ya mbaazi hutumika kama chakula kwa ajili ya kulishia
mifugo.
Hali ya hewa
Mbaazi hustawi vizuri katika nyuzi joto 29 hadi 38, na
hupandwa kuanzia usawa wa bahari hadi mita 1900 kutegemeana na aina ya mbegu.
Kuna mbegu zinazostawi katika ukanda wa chini, wa kati na wa juu. Aidha kuna
aina zinazostawi zaidi ya mita 2000 kutoka usawa wa bahari Zao hili huhitaji
kiasi cha milimita 600 hadi 1000 cha mvua kwa mwaka. Aina za mbaazi za muda
mfupi hutosha kustawi katika mvua kiasi cha milimita 250 hadi 370 kwa mwaka.
Udongo
Kwa kilimo chenye tija, ni vizuri kuotesha mbaazi kwenye
udongo unaoruhusu maji, wenye mbolea kiasi na wenye tindikali kiasi cha pH
kuanzia 5 hadi 7.
UTAYARISHAJI WA
SHAMBA.
• Shamba la mbaazi litayarishwe mapema kwa kung’oa mabaki
yote ya mimea pamoja visiki kabla ya kulilima.
• Lima shamba kiasi kisichopungua sentimeta 30.
• Lainisha udongo kwa kupitisha haro.
• Tayarisha matuta au makinga maji kama shamba liko kwenye
mteremko.
Kuandaa mbegu
• Mbegu bora iliyochaguliwa vizuri na kuhakikiwa kiwango cha
uotaji ziandaliwe.
• Mbegu ziwekewe dawa ya kuzuia kuvu (fungus) kabla ya
kupanda ili kuzuia magonjwa yatokanayo na mbegu na udongo.
Mbegu bora
Mbegu za mbaazi zimegawanyika katika makundi makubwa matatu
nazo ni, mbegu za muda mfupi, mbegu za muda wa kati, mbegu za muda mrefu.
KUPANDA.
1. Mbaazi za muda
mfupi, zipandwe peke yake bila kuchanganya na mazao mengine. Nafasi: Kuwe na nafasi ya sentimeta 75
toka mstari na mstari, sentimita 20 toka shimo hadi shimo. Kiasi cha mbegu: Kilo 5 hadi 6 zaweza kutumika kwa ekari moja.
2. Mbaazi za muda wa
kati, zipandwe peke yake na katika mwinuko kutoka usawa wa bahari wa mita 1000
hadi 1880 Nafasi: Kuwe na nafasi ya
sentimita 120 toka mstari hadi mstari na sentimita 30 toka shimo hadi shimo. Kiasi cha mbegu: Waweza kutumia kilo 5
kwa ekari moja.
3. Mbaazi za muda mrefu, zipandwe peke yake katika mwinuko
toka usawa wa bahari wa mita 1000 hadi 1880. Nafasi: Kuwe na sentimita 150 toka mstari hadi mstari na sentimita
50 toka shimo hadi shimo. Kiasi cha
mbegu: Waweza kutumia kilo 5 kwa ekari moja
PALIZI NA KUPUNGUZIA
MIMEA.
Ni muhimu kupalilia mapema (angalau mara mbili kulingana na
kiasi cha unyevu au mvua) na kuondoa magugu ambayo hushindana na mimea
michanga. Miche ikiwa mingi kwenye shina husababisha mazao kuoza. Kwa hivyo ni
muhimu kupunguza miche na kubaki miwili au kutegemeana na nafasi.
WADUDU.
Kuna wadudu wa aina
mbalimbali ambao kushambulia mbaazi, wakati zikiwa shambani au zikiwa galani.
1. Vidukari
Vidukari weusi wanaotembea kwa
makundi na ambao huonekana zaidi katika sehemu changa za mimea kama vichomozo,
matawi na majani. Wadudu hawa husambaa kwa wingi wakati wa majira ya ukame.
Wadudu hawa hufyonza majimaji au utomvu ulio kwenye maeneo hayo na kusababisha
mbaazi kubadilika rangi na kukauka. Udhibiti….Wadudu
hawa hudhibitiwa kwa kutumia njia bora za kilimo na kufanya kilimo cha
mzunguko.
2. Kunguni wa mifuko ya mbaazi
Kuna aina nne za wadudu hawa ambao
ni Kunguni wa kahawia (Claiigralla spp), Kunguni wakubwa (Anoploenemies spp),
Riptutasi (Riptortus dentipes), Kunguni wa kijani (Nezara viridula). Wadudu
hawa hufyonza mbegu inayokuwa kupitia kuta za mifuko na kufanya mbegu kuoza na
kukosa thamani ya kuwa mbegu na chakula cha binadamu. Udhibiti….Wadudu wanaofyonza mifuko ni vigumu kuwadhibiti kwani
huruka kutoka sehemu moja na kwenda nyingine hivyo wanaweza kukusanywa kwa
chandarua na kuangamizwa.
3. Mbawakavu wa maua na chavua (Blister
beetles)
Wadudu hawa wenye rangi ya njano
hula maua na kupunguza uzalishaji wa mifuko ya mbaazi. Katika eneo ambalo
uzalishaji wa mbaazi ni mkubwa, wadudu hawa hufanya uharibifu mdogo kuliko
katika eneo ambalo mbaazi huzalishwa kwa kiasi kidogo. Udhibiti….Wadudu hawa wanaweza kudhibitiwa kwa kuwaondoa kwa mikono
na kuwauwa isipokuwa wakati wa kuwashika kuwepo na uangalifu kwani
wakisumbuliwa huweza kutoa kemikali ambayo inaweza kuunguza mikono au mwili.
4. Funza wa vitumba (Maruca vitrata)
Wadudu hawa hutaga mayai kwenye vikonyo vya mbaazi kabla ya kuchanua au
juu ya mifuko hula vikonyo vya maua na mbegu iliyoko ndani ya mifuko ya mbaazi.
Udhibiti….Mkulima anaweza
kuwadhibiti wadudu hawa kwa kufanya ukaguzi wa shamba mara kwa mara ili
kufahamu uwepo wa wadudu hawa, pamoja na kutumia viuatilifu kulingana na
maelekezo ya mtaalamu wa kilimo. Ni vyema ukaguzi ukafanyika wiki moja kabla ya
mbaazi kuchanua na baada.
5. Inzi wa mifuko (Melanagromyza chacosoma)
Hawa ni wadudu wadogo weusi warukao na wanaotaga mayai katika kuta za
mifuko za mbaazi inavyokua. Funza wake ni weupe na wana urefu wa sentimeta 3.
Wadudu hawa hufanya uharibifu mkubwa kwa kula mbegu changa iliyopo kwenye
mifuko. Udhibiti….Katika maeneo
ambayo wadudu warukao ni tatizo, jamii ya mikunde inayokomaa kwa muda tofauti
isipandwe kwenye shamba moja ili kuzuia mwendelezo wa kuzaliwa kwa inzi hawa
hasa kila aina ya mikunde inapotoa maua. Pia mwarobaini waweza kunyunyiziwa
mara 4 kila baada ya wiki kwa kiwango cha gramu 50.
6.
Vithiripi
(Megalurothrips spp. And Frankliniella schultzei)
Wadudu hawa wadogo na wenye rangi ya kahawia na mabawa ya njano huathiri
mbaazi hasa kwa kufyonza utomvu kwenye majani na maua.Husababisha maua na
vikonyo kusinyaa, kufifia rangi na kudondoka kabla ya kukomaa. Udhibiti….Kagua shamba kila mara ili
kufahamu uwepo wa wadudu hao kabla ya mimea kuchanua ili kudhibiti mapema.
7.
Vipekeche
Hawa ni wadudu wanaoshambulia mbaazi ikiwa
ghalani. Wadudu hawa hutoboa mbegu na kutengeneza mashimo ya kutokea wadudu
kamili.
No comments:
Post a Comment